Na, Edigar Nkilabo – SikongeDC
Washiriki wa mafunzo kwa vitendo kutoka chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC) wamefanya ziara Wilayani Sikonge katika kiwanda cha kati cha kuchakata na kufungasha mazao ya nyuki kwa lengo la kujifunza kwa vitendo utekelezaji wa sera za serikali katika shughuli mbalimbali za maendeleo nchini.
Awali Washiriki hao wa Mafunzo ya Vitendo - NDC, waliwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Sikonge kujitambulisha na kueleza lengo kuu la ziara hiyo ya kikazi.
Akizungumza kwa niaba ya Washiriki wa Chuo hicho, Kaimu Mkuu wa NDC Brigedia Jenerali Charles Ndiege amesema lengo la ziara hiyo ni kujifunza kwa vitendo namna Wilaya ya Sikonge inavyotekeleza sera za serikali katika uzalishaji hasa kwa kutumia rasilimali zilizopo.
"Kupitia ziara hii tutapata ujuzi na uzoefu utakaowasaidia Washiriki wa Mafunzo kuchambua kwa kina utekelezaji wa sera za serikali na kuishauri njia bora za uboreshaji wa shughuli za maendeleo katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa"alisema Brigedia Ndiege.
Aidha Brigedia Ndiege ameipongeza Halmashauri kwa ubunifu wa kuanzisha kiwanda cha kati ambacho kimeongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya nyuki pamoja na kufungua milango ya ajira kwa vijana na wakazi wa wilaya ya Sikonge.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe.Thomas Myinga amesema kiwanda hicho kimechangia kuongeza mapato ya Halmashauri na kuhakikisha uwepo wa soko la ndani na nje ya nchi.
" Wilaya yetu ya Sikonge ni kubwa ina eneo la hifadhi la kutosha moja ya shughuli zinazofanywa na wananchi ni kulina asali, kiwanda hiki kimechochea ushiriki wa wananchi katika uzalishaji wa asali ambapo kwasasa Wananchi 6000 wanajishughulisha na uzalishaji wa mazao ya nyuki"alisema Mhe.Myinga.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Ndg.Seif Salum amesema maoni na ushauri uliotolewa na Washiriki wa Mafunzo kwq Vitendo NDC wataufanyia kazi ili kuongeza tija na manufaa kwa Wananchi na serikali.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa