WANANCHI JITOKEZENI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA.
SIKONGE Wananchi wahimizwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura mara muda utakapotimia.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Mhe. Peter Nzalalila alipokuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za maadhimisho ya Serikali za Mitaa Wilayani hapa yaliyofanyika katika Kata ya Mkolye na kuhuzuliwa na viongozi mbalimbali wa ngazi ya Wilaya pamoja na wataalamu wa Halmashauri.
Katika serehe hizo Mhe. Nzalalila alisema kuwa hivi sasa serikali inaelekea katika uchaguzi mdogo wa wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji hivyo basi ni vyema jamii ikajiandaa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo muhimu.
“serikali inaanzia ngazi za vitongoji kwenda mpaka juu tunapompata Waziri mwenye dhamana ambaye ni Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)” alifafanua ili kuwapa picha halisi ya namna uchaguzi huo ulivyo muhimu.
Aidha alitoa hamasa kwa wananchi kujiandaa na uchaguzi huo kwa kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia uboreshwaji wa daftari hilo.
Umati wa Wananchi wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi Mhe.Nzalalila (hayupo pichani) siku ya maazimisho ya Serikali za Mitaa Mkolye.
“wakati utakapofika wote tujitokeze kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ili tupate haki yetu ya msingi ambayo ni kumchagua kiongozi bora anayefaa kutuongoza kwa miaka mitano ijayo” alisema.
Awali Diwani wa kata ya Mkolye Mhe. Seif Mayoka alisema kuwa hali ya kisiasa katika kata hiyo ni nzuri na wananchi wana imani kubwa kwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutokana na kutekeleza vyema ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 kama ilivyoahidi. Aliongeza kuwa wana Mkorye hawataiangusha serikali yao katika uchaguzi ujao wa serikali za Mitaa ambao utafanyika nchi nzima.
Maadhimisho ya Serikali za mitaa hufanyika kila tarehe moja ya Mwezi wa Saba ambapo Wilayani Sikonge huadhimisha sherehe hizi kwa burudani mbalimbali na wananchi hupata fursa ya kusikiliza kutoka kwa viongozi mbali mbali namna serikali inavyotekeleza kwa upande wa Serikali za Mitaa.
TEHAMA SIKONGE
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa