WAHESHIMIWA MADIWANI SIKONGE WAPATA MAFUNZO
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, ndugu Seleman Pandawe ameandaa mafunzo kwa waheshimiwa Madiwani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo Cha Maendeleo Sikonge (FDC) kwa siku mbili kuanzia tarehe 19 hadi 20 Novemba 2021.
Mafunzo hayo yameshirikisha taasisi mbalimbali katika kutoa mafunzo kwa Madiwani na Wakuu wa Idara, wakiwemo TAKUKURU, Mahakama, Polisi, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda, Ofisi ya RAS pamoja na chuo cha Uhazili Tabora.
Akifungua mafunzo hayo Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, amesisitiza umakini na utulivu ili tufaidike na mafunzo hayo muhimu Kwa ajili ya kuendesha Halmashauri yetu kwa kufuata Sheria na taratibu zilizopo.
Akitoa mafunzo Wakili wa Mahakama ya Mwanzo Bi. Winfrida Magai alishauri tupende kujisomea sheria ili kuwa na uelewa kwa baadhi ya mambo na pia kufahamu mabadiliko ya sheria ambayo hutokea. Pia ameeleza taratibu za kufuata pindi unapotaka kufungua kesi pamoja na vitu vinavyohitajika kwenye baadhi kesi mfano kesi za mirathi.
Nae, Mtaalam kutoka Chuo cha Uhazili, ndugu Brevius Ludovic alitoa mafunzo juu ya Kazi, Wajibu na Majukumu ya Diwani pamoja na misingi ya usimamizi wa fedha na taratibu za manunuzi. Pia aligusia kuhusu mbinu za Menejimenti na Uongozi katika Utawala wa kidemokrasia.
Aidha, Mtaalam kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ndugu Onesmo Msalangi alitoa somo kuhusu uzingatiaji wa kanuni za Maadili ya Waheshimiwa Madiwani ya Mwaka 2000 lakini pia alitoa mafunzo ya dhana ya mgongano wa Maslahi Kwa Madiwani na Viongozi wa Umma.
Mada juu ya Taratibu za Mikutano na uendeshaji wa shughuli za Halmashauri (Vikao na Mikutano) ilitolewa na Afisa Utumishi na Utawala ndugu Nico Kayange akishirikiana na Afisa Sheria ndugu Paschal Kapinga. Nae Mtaalam kutoka TAKUKURU Bi. Ilandike Lucas alitoa Elimu juu ya kuzuia na kupambana na Rushwa halikadhalika Muwakilishi wa OCD Kamanda Isp. Mdoe Waziri alitoa mafunzo juu ya ulinzi na usalama. Na Mtaalam kutoka ofisi ya RAS ndugu Siame Mbati alitoa Mada ya hatua za kinidhamu kwa Watumishi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Mhe. Rashid Magope kwa niaba ya Madiwani wote aliwashukuru wawasilishaji wa Mada zote kwa uwasilishaji mzuri na unaoeleweka. Kwa ujumla mafunzo yalikuwa mazuri na yenye kushirikisha ambapo wajumbe waliweza kuuliza maswali, kujadili na kupata ufafanuzi.
Nae, Mbunge wa Jimbo la Sikonge, Mhe. Joseph Kakunda alipata kushiriki mafunzo na kueleza baadhi ya mambo hasa juu ya Sheria na Taratibu pia aliuliza swali Kwa watoa Mada wote akihoji neno Bahati mbaya huweza kuchunguzwa vipi? akitoa mfano wa stori ya Dereva na Bosi wa sehemu fulani kilichowakuta, swali ambalo lilifafanuliwa vizuri na Mtaalam kutoka ofisi ya OCD na pia Mtaalam wa TAKUKURU.
Aidha, Mhe. Kakunda ambae pia alikuwa mshiriki alipewa nafasi ya kufunga mafunzo hayo na kuchua nafasi kuwashukuru walioandaa mafunzo na kushauri siku nyingine yafanyike kabla ya kuanza mabaraza ili kujinoa juu ya uendeshaji wa shughuli za Halmashauri na usimamizi wa Miradi Kwa ujumla. Aliongeza kwa kusema kuwa wamejifunza juu ya uhusiano wa Serikali na mihimili kama Polisi, Mahakama na TAKUKURU.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa