TULU IMENICHEFUA-MHE. ANTONY MAVUNDE
Ziara ya Naibu Waziri ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu, Mhe Antony Mavunde imeingia doa leo baada ya kupata taarifa iliyomchefua ya kituo cha vijana maarufu kama TULU kilichopo katika Kata ya Igigwa Wilayani Sikonge.
Kituo hicho cha vijana ambachokilikuwa na lengo zuri kwa maendeleo ya vijana katika Wilaya ya Sikonge kimewanufaisha vijana wachache kwa miaka mitano ukilinganisha na makusudio yake pia kingeweza kuwapa vijana ujuzi na maarifa ambayo wangeyatumia kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali na kuziuza ndani ya Wilaya na hata nje.
Aidha, Mhe. Antony Mavunde ameeleza,”hii ni Halmashauri ya kwanza kubuni mradi kama huu wenye manufaa kwa jamii na nchi kwa ujumla lakini hamjakitendea haki kituo na vijana wa Sikonge kwa ujumla…bado haitoshi kituo kilichotumia fedha nyingi za wananchi zaidi ya bilioni 1.5 kinaenda kusajiliwa kama NGO…Tunaenda kufukua makaburi na waliohusika hatutawaacha hivi hivi”. Amemuagiza DC Sikonge kuunda tume ndogo itakayochunguza thamani ya fedha iliyotumika kwenye mradi huo.
Pia Mhe. Mavunde alisisitiza juu ya kituo hicho kuwa kitengenezewe utaratibu mzuri haraka utakao wanufaisha vijana wa Sikonge bila kuwaacha wale vijana walioanzisha kituo hicho kwani kitakuwa kituo cha mfano kwa nchi yetu.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri pia amepata fursa ya kuongea na wananchi hasa vijana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Sikonge eneo la madukani na kuwaahidi kuwaletea mpango wa kurasmisha ujuzi wa vijana ambao umeshaanza kwa baadhi ya maeneo nchini na upo chini ya ofisi yake.
Aidha, Mhe. Mavunde amewataka vijana kujiunga katika vikundi na kuchagua viongozi watakao kuwa waadilifu ili waweze kukopeshwa na kuendesha miradi itakayowainua kiuchumi. Pia amesisitiza kuwa fedha hizi za mikopo hazina miguu yaani hazimfuati mtu, zinapatikana kwa utaratiu alioueleza awali. DC Sikonge, Peres Magiri baada ya kusikia habari ya SACCOS ambayoinaweza kupata mkopo kutoka ofisi ya Mhe. Mavunde alimpa Mkurugenzi Mtendaji Sikonge, Dakt. Simon Ngatunga mwezi mmoja awe amekamilisha uundaji wa SACCOS ya vijana na kutuma maombi ya mkopo haraka ili vijana wa Sikonge wanufaike.
Kabla kuhitimisha mkutano wa hadhara Mhe. Mavunde aliwashukuru wananchi wa Sikonge kwa kujitokeza kwa wingi pia aliwapongeza kwa kumchagua Mbunge wa Sikonge ambae sasa ni Naibu Waziri OR TAMISEMI, Mhe. Joseph Kakunda mchapa kazi mahiri na mtu wa vitendo tu sio maneno mpaka anatamani angekuwa mpiga kura wake kwa maendeleo anayoyaleta Sikonge ikiwemo miradi ya barabara, Maji ya ziwa viktoria, Miradi ya Elimu na Hospitali ya Wilaya na kuwataka wasiipoteze bahati hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa