SIKONGE YAJIPANGA KUKUSANYA MAPATO 100% KWA MWAKA WA FEDHA 2019/2020
Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge yaendesha semina elekezi kwa Watendaji wa Kata na Vijiji iliyolenga kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka 87% iliyokusanywa kwa mwaka wa fedha 2018/2019 hadi kufikia 100% kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Semina hiyo itakayofanyika kwa muda wa siku mbili (2) kuanzia tarehe 13 mpaka tarehe 14/8/2019 imeandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Bi. Martha Luleka ikiwa na lengo la kuweka mikakati ya pamoja kati ya utawala na watendaji hao itakayowezesha ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri ya Sikonge kufikia 100% sanjari na kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato vitakavyotumika ili kufikia lengo hilo.
Pia semina hiyo iliwakutanisha watendaji pamoja na Viongozi mbalimbali Wilayani hapa na kufunguliwa na mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Mhe. Peres Magiri aliyewataka watendaji hao kusimamia vyema vyanzo vya mapato katika kata wanazozitumikia kwani watendaji ndio msingi wa kusimamia mapato ndani ya Halmashauri ikiwa watajua vyema wajibu walionao.
Akiongea wakati wa Ufunguzi wa semina hiyo Mhe. Magiri alitolea mfano kuwa miradi mikubwa inayotekelezwa nchini, chini ya uongozi wa serikali ya awamu ya tano kwa asilimia kubwa imetokana na mapato ya ndani ya nchi ambayo yamesimamiwa vizuri ikiwemo kodi mbalimbali zilizokusanywa na kuwasilishwa kwa uaminifu. Aliongeza kuwa jambo hili limewezekana kutokana na kuwepo kwa nidhamu ya matumizi ya fedha. Hivyo basi amewataka watumishi wa Sikonge kuwa na nidhamu ya fedha pamoja na kuwasilisha mapato kwa uaminifu ili Halmashauri iweze kufikisha 100% iliyojiwekea.
Watendaji Kata na Vijiji wakifuatilia mafunzo toka kwa Mkurugenzi Bi. Martha Luleka aliyesimama.
Kuntu ya hayo pia mambo mbalimbali ya kimkakati yalijadiliwa katika semina hiyo huku Mbunge wa Sikonge, Mhe. Joseph Kakunda mbaye alikuwa ni miongoni mwa wazungumzaji akiwataka watendaji hao kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi ikiwemo kuzifahamu kero zinazowakabili wananchi wao na kuweka mbinu za utatuzi wa kero hizo kwa kuwashirikisha wananchi.
Wajumbe pia walipata wasaa wa kusikililiza salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo ziliwasilishwa na Mdau wa Maendeleo Ndugu. Jeff Kisangaye kutoka ofisi ya Rais Dawati la Siasa ambaye alisisitiza kuwa watendaji wajenge mahusiano mazuri na wadau watakaochangia maendeleo katika Kata na Wilaya kwa ujumla.
Aidha, wakati wa kuhitimisha semina elekezi Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Martha Luleka aliwataka watendaji hao kuwa viongozi wenye kuleta matokeo chanya, huku akisisitiza kuwa hawatakubali kuwa wa mwisho kimapato hivyo wanasikonge wote waungane kupambana kimaendeleo mpaka mafanikio yapatikane.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa