SERIKALI YA AWAMU YA SITA IMEDHAMIRIA KUWALETEA MAENDELEO YENYE TIJA.
SIKONGE,
8.10.2021.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt.Batilda Buriani amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inalenga kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora za jamii pamoja na kuwasaidia kujikwamua kiuchumi ikizingatiwa kwamba Tanzania ipo katika uchumi wa kati.
Balozi Batilda ameyasema hayo alipofanya mkutano wa Hadhara Wilayani Sikonge Mnadani akihamasisha Chanjo ya UVIKO-19.
“Ndugu zangu naomba niwaeleze Serikali hii makini inataka kila Mtanzania aweze kufaidi uchumi wa kati,tunaposema uchumi wa kati tumaanisaha kila mmoja ajumuike,Mhe.Raisi anataka uchumi jumuishi asiachwe mtu nyuma, awe ni mfugaji, awe mama ntiliye, awe anaejihusisha na kilimo…kila mmoja katika shughuli anayoifanya tuhakikishe tunawashika mkono na wanaweza kufaidika na uchumi wa kati” Balozi Batilda alifafanua zaidi.
Aidha,Balozi Batilda ameitaja miradi mbalimbali ambayo Serikali ya awamu ya Sita imetekeleza na inaendelea kutekeleza kwa wananchi akisema Takribanui Bilioni 8 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara vijijini katika Mkoa wa Tabora mwaka (2020), huku bilioni 26 kwa mwaka huu 2021 zikitolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara zikiwemo barabara za Sikonge na kuongeza kuwa mradi wa maji kutoka ziwa Viktoria unaendelea kutekelezwa ili wananchi wa Sikonge na maeneo mengine wapate maji safi na salama.
Sambamba na hilo Dkt.Batilda amesema Serikali imejielekeza kujenga vituo vya afya vya kisasa ambavyo vitatoa huduma za afya kwa wananchi na kuongeza kuwa Mkoa wa Tabora umepokea Tsh.Bilioni 1.5 ikiwa ni sehemu ya tozo za miamala ambazo zimeelekezwa kujenga(kukamilisha) ujenzi wa vituo vya afya.
“Tarafa zetu zote zitakuwa na vituo vya Afya, na vituo vya afya kipindi hiki sio vile vya zamani..leo kituo cha afya ni sawa na umepata hospitali, kina eneo la wagonjwa wa nje ,kina wagonjwa wanaolazwa, kina wodi ya akina baba,mama na Watoto vilevile kina kitengo cha upasuaji mkubwa na upasuaji mdogo.” Dkt.Batilda amefafanua.
Na.Anna Kapama.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa