Maadhimisho ya sherehe za MEI MOSI 2018 Wilayani Sikonge yamefanyika katika Kata ya Sikonge eneo la kiwanja kipya cha mpira wa miguu karibu na soko la TASAF ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Bwa. Peres Magiri.
Katika sherehe hizo, Mwaka huu Wilayani Sikonge zimeratibiwa na Chama cha Wafanyakazi TUGHE ambapo ni kawaida ya vyama hivi hapa Wilayani kubadilishana kila Mwaka katika kuratibu zoezi zima la sherehe.
Aidha, sherehe hizo zilianzia katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa maandamano ya wafanyakazi wote pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi Mbirani waliotumbuiza kwa nyimbo na ngoma katika msafara kuelekea uwanjani.
Mgeni rasmi alipanda jukwaani kwa ajili ya hotuba baada ya kupokea risala iliyosomwa na muwakilishi kutoka TUGHE Bwa. Gerald Mwagalazi, risala hiyo ilikuwa na malalamiko mbalimbali ya watumishi ikiwemo madai ya likizo za watumishi.
“Awamu hii ya tano ya Rais wetu Mhe. John Pombe Magufu imelenga kuibadilisha Tanzania na dalili zote zinaonesha kuwa mambo yanaenda kuwa bamu bamu” alisema hayo mgeni rasmi.
Aidha, aliwapongeza wafanyakazi kwa namana ya pekee kwa jitihada wanazozifanya katika kuleta maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla. “ Mataifa makubwa yaliyoendelea yamefika hatua hiyo kwa jitihada kubwa za wafanyakazi katika kutimiza wajibu wao, ni imani yangu kuwa wafanyakazi mtasimama imara kuhakikisha mnalitumikia Taifa letu kwa bidii na nguvu zenu zote ili kuhakikisha tunasonga mbele” alisisitiza mgeni rasmi.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Dakt. Simon Ngatunga aliwataka viongozi wa vyama vya wafanyakazi kuwawakilisha ipasavyo wale waliowachagua. “Inashangaza wafanyakazi bora wa Mwaka 2015/2016 hawajalipwa mpaka leo, na leo ninapata taarifa jukwaani kwamba kuna hawa hawakulipwa…nyinyi ni kiunganisho kati ya mimi mwajiri na watumishi hawa, mje tukae chini tutatuwe kero hizo na sasa wale wote nilioletewa majina yao hapa, kesho waje ofisini wachukue pesa zao” alisema Mkurugenzi.
Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Mhe. Peter Nzalalila alitoa agizo katika sherehe hizo, kuwa robo ya pili ya Mwaka ujao waletewe mkakati wa maandalizi katika kikao cha baraza la Madiwani baada ya kuona maandalizi ya sherehe za Mwaka huu hayakuwa vizuri sana. “Kwa sababu sisi wananchi tunawategemea sana wataalam wetu, pia maendeleo yanategemea wao… Sasa tukionekana kama hatuwaonioni hivi haipendezi” alisema Mwenyekiti huyo.
Sherehe hizo zilihitimishwa kwa kutoa vyeti kwa wafanyakazi bora kutoka katika kila idara na zawadi za fedha ambazo zitaingizwa katika akaunti zao moja kwa moja kupitia mfumo mpya wa malipo wa TISS ambao umeanza kutumika wiki hii.
IMEANDALIWA NA KITENGO CHA TEHAMA
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa