Maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu (TB) Duniani yamefanyika jana Kimkoa katika Kata ya Kitunda maeneo ya Mgodini Wilayani Sikonge ambapo Mgeni Rasmi akiwa ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Mhe. Peter Nzalalila.
Mratibu wa TB Mkoa wa Tabora, Benedict Komba alitoa historia ya maadhimishi hayo kuwa yalianza mwaka 1882 baada ya kugundulika kwa vimelea vya ugonjwa wa TB, ndipo ikawa siku ya maadhimisho ya ugonjwa wa TB Duniani kote. Pia alieleza kuhusu Kauli mbiu ya Mwaka huu kuwa, Viongozituwe mstari wa mbele kupambana ili kutokomeza Kifua Kikuu. Mratibu huyo alieleza kuwa takwimu zinasema kwa kila kundi la watu Laki Moja kuna wagonjwa 327 wa Kifua kikuu, hivyo ugonjwa huu ni hatari sana.
Nae mratibu wa TB Wilaya ya Sikonge, Dr. Buswelu alitoa taarifa ya zoezi zima la upimaji ambapo watu zaidi ya 753 walikuwa wamepima HIV na watu 134 walikuwa wamepima TB na 6 kati yao walibainika kuwa na vimelea vya TB, hivyo walianza kupata tiba. Mpaka zoezi linaisha watu 922 walikuwa wamepima HIV, 17 kati yao walikuwa na Virusi na kwa upande wa TB watu 196 walichunguzwa, 7 kati yao walikuwa na TB.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wilaya, Venance Ngeleuya aliwaeleza wananchi kuwa wanapoona dalili zinazoendana na ugonjwa wa TB, wafike haraka katika vituo vinavyotoa huduma ya TB. " Msiogope kwenda kupima kwa kuwa baadhi ya dalili za TB zinafanana na dalili za UKIMWI basi mtu unafikiri ni UKIMWI bila hata kupima...," alisema Kaimu huyo.
Aidha, mgeni rasmi alitoa agizo la kuanzisha huduma ya vipimo na tiba ya TB katika Zahanati ili kupeleka huduma karibu na wananchi. Alisema hayo baada ya kuona kuwa huduma hiyo inatolewa katika Vituo vinne tu Wilaya nzima. " Naagiza kuanzia Mwezi ujao vituo nane vianze kutoa huduma hiyo huku Mganga Mkuu Wilaya anaandaa utaratibu ili Zahanati ikiwezekana zote ziwe zinatoa huduma hiyo," alisema mgeni rasmi.
Pia, mgeni rasmi alisema kuwa eneo la mgodi wa Kitunda linawatu wengi sana wanaotoka sehemu mbalimbali lakini huduma ya matibabu iko mbali sana. Aliwaita mbele viongozi wa wachimbaji madini na Mtendaji wa Kata hiyo kisha akasema, "wiki ijayo mniletee mpango mkakati wa kuanza ujenzi wa Zahanati katika mgodi huu na wananchi hapa wako tayari kwa hilo, au sio jamani!?" wananchi walifurahi na kusema wako tayari kwa hilo. " Mtendaji hiki ni kipimo chako cha kuendelea kuwepo hapa Kitunda, vinginevyo Nyahua itakuhusu" alisema Mhe. Nzalalila.
Baada ya Mtendaji huyo kuambiwa kuwa atahamishiwa Kata ya Nyahua endapo atashindwa kufanikisha ujenzi wa Zahanati mgodini, mgeni rasmi alitembelea mabanda yaliyokuwa yanatoa huduma ya vipimo na kuridhishwa na zoezi hilo.
Kabla ya kuanza maadhimisho, Mwenyekiti alipata fursa ya kutembelea mradi wa Ujenzi wa Wodi ya Mama na Mtoto, Maabara na Nyumba ya Mganga katika Kituo cha Afya Kitunda. Wodi hiyo ipo katika hatua ya Msingi, nyumba ya Mganga ipo hatua ya lenta na Maabara msingi umekamilika.
Aidha, Mkandarasi anaesimamia ujenzi huo aliahidi kuwa mpaka kufikia tarehe 30 Mei 2018 ujenzi utakuwa umekamilika kwa Majengo yote matatu (3). Akizungumza Mhandisi huyo alisema,
" Changamoto kubwa iliyotupata ni kubadilika kwa mchoro wa ramani ya jengo la wodi ya mama na mtoto wakati ambapo ujenzi ulikuwa umeshaanza."
Mwenyekiti Nzalalila alichukizwa sana na gharama kubwa anayolipwa fundi huyo na kusema, " hii sio maana halisi ya 'Force Account', kwa sababu gharama ni kubwa mno, zaidi ya Milioni 10 kwa jengo moja analipwa ' local' fundi." Baada ya kusema hayo alitoa agizo kwa Viongozi na wataalam kuwa jambo kama hilo lisijirudie tena katika Halmashauri hii.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa