Kaimu Mkurugenzi Mtedaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Bw. Bwenge Mwesigwa ameongoza timu ya menejimenti kukagua miradi inayopendekezwa kufikiwa na mbio za mwenge wa uhuru mwaka huu 2024.
Kati ya miradi iliyokaguliwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa kisima kirefu cha pampu ya umeme chenye urefu wa mita 101 katika shule ya msingi Muungano iliyopo kata ya Mole.Mradi huu una gharama ya kiasi cha shilingi milioni 45 , kisima hiki kikikamilika kina uwezo wa kutoa lita za maji 14,500 kwa saa.Mradi umefika asilimia 60% na tayari mkandarasi wa mradi huu yupo katika hatua za mwisho za kuanza kazi ya umaliziaji wa kisima hicho.
Mradi mwingine uliokaguliwa na menejimenti ni ujenzi wa kituo cha afya Igigwa kilichopo kata ya igigwa chenye thamani ya shilingi milioni 332.8.Mradi huu unahusisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD),maabara,shimo la kutupia kondo la nyuma ,vyoo vya nje pamoja na kichomea taka,mradi wa ujenzi umefikia asilimia 95%.
Vilevile menejimenti imezuru shule ya sekondari Kamagi kukagua mradi wa ujenzi wakuongeza miundombinu ya kidato cha tano na sita,uliopo kata ya Misheni,mradi huo unahusisha ujenzi wa vyumba 9 vya madarasa,mabweni 4 pamoja na ujenzi wa matundu 14 ya vyoo.Mradi unagharimu shilingi milioni 808 na mradi umekamilika.
Mradi wa mwisho uliotembelewa na menejimenti ni mradi wa vijana wa ushonaji wa nguo,uliopo eneo Sikonge madukani,kata ya Sikonge,mradi unagharama ya shilingi milioni 16 ikiwa ni mkopo wa kuwakwamua vijana kiuchumi toka halmashauri unaohusisha vijana 05,mradi unaendelea vizuri.
Akijumuisha ukaguzi huo Kaimu mkurugenzi ameagiza ukamilishwaji wa miradi kwa haraka hususani mradi wa kisima kirefu cha maji katika shule ya msingi Muungano na kusafisha maeneo yote yanayozunguka eneo la ujenzi wa kituo cha afya Igigwa.
Aidha amemuagiza mweyekiti wa kikundi cha vijana cha ushonaji wa nguo kuwasilisha taarifa ya marejesho ya kikundi hicho pamoja na stakabadhi za malighafi zote walizonunua kiwandani hapo.
Ziara hii ni maandalizi ya mbio za mwenge wa uhuru 2024 ambazo zilizinduliwa rasmi Aprili 2, 2024 mkoani Kilimanjaro na zinatarajiwa kufika mkoani Tabora Agosti 16, 2024,zikiongozwa na kauli mbiu isemayo “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu”.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa