Elimu juu ya lishe, tiba pamoja na chanjo zimetolewa leo na wataalam toka Halmashauri ya wilaya ya Sikonge divisheni ya kilimo na mifugo. Ni katika zoezi la maadhimisho ya siku ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa duniani,yanayofanyika katika viwanja vya Mnadani pamoja na viwanja vya Shule ya Msingi Sikonge.
Zoezi hili limeendeshwa vyema na Maafisa toka divisheni ya Kilimo na Mifugo ,Gelard Mwagalazi pamoja na Phildorine Linus katika viwanja vya mnadani.Bw. Mwagalazi akizungumza na wateja waliofika kupata elimu na chanjo kwa ajili ya mbwa wao amesema ni vema wamiliki wa mbwa kuhakikisha kuwa wanawapatia mbwa wao chanjo ya kila mwaka kwa tarehe na mwezi husika ili kuwakinga mbwa wao dhidi ya ugonjwa hatari wa kichaa cha mbwa.
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge,Mkuu wa Divisheni ya Kilimo na Mifugo Ndugu Hashim Kazoka ameridhishwa na mwamko wa wananchi wa Sikonge kwa kuja kupata elimu na chanjo kwa ajili ya kuwakinga mbwa wao dhidi ya ugonjwa hatari wa kichaa cha mbwa.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa wanao fuga mbwa kuzingatia lishe na tiba ikiwa ni pamoja na kuwapatia dawa za minyoo,kuwaosha na kuwafungia ndani.Matarajio yake ni kumaliza dozi zote mia tatu(300) walizopatiwa ndani ya siku mbili za maadhimisho ya siku ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa duniani.
Zoezi hili ni endelevu hata baada ya siku ya kesho tarehe 28/09/2023 ambayo ndio kilele cha siku ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa duniani.
Maadhimisho haya ni ya 16 tangu kuanzishwa kwa siku ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa duniani mwaka 2007 ili kuinua ufahamu juu ya ugonjwa hatari wa kichaa cha mbwa duniani.Takwimu toka Kituo cha kudhibiti magonjwa duniani ,zinasema takribani watu elfu sitini hufariki kila mwaka kutokana na ugonjwa hatari wa kichaa cha mbwa kote duniani.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa